Habari

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dkt. Charles Msonde mapema leo

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dkt. Charles Msonde mapema leo

Jumla ya watumishi wa umma 14,409 wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi na watumishi 1,907 hawajawasilisha vyeti kwa ajili ya kuhakikiwa licha Serikali kutoa muda wa kutosha kwa watumishi hao kuwasilisha vyeti vyao Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwa ajili ya uhakiki.

Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dkt. Charles Msonde mapema leo wakati akiwasilisha taarifa ya sita na ya mwisho ya zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma vya ufaulu wa kidato cha Nne, cha Sita na Ualimu kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI Dkt. Laurean Ndumbaro.

Dkt. Msonde amesema katika awamu ya sita jumla ya watumishi 5,696 wamehakikiwa vyeti vyao, kati ya hao, watumishi 5,404 sawa na asilimia 94.82 wamebainika kuwa na vyeti halali na watumishi 295 sawa na asilimia 5.518 wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi.

Aidha, Dkt. Msonde amefafanua kuwa, jumla ya watumishi wa umma 511,789 wamehakikiwa katika awamu zote sita za uhakiki, kati ya hao watumishi 494,554 sawa na asilimia 96.71 vyeti vyao vimebainika kuwa ni halali, watumishi 14,409 sawa na asilimia 2.82 wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi na watumishi 1,907 hawajawasilisha vyeti vyao ili vihakikiwe.

Pia, Dkt. Msonde amesema Ofisi yake imebaini kuwa watumishi 71 majina yao halisi waliyoajiriwa nayo ni tofauti na majina katika vyeti walivyotumia kujipatia ajira katika Utumishi wa Umma. Ameeleza kuwa Ofisi yake ilichukua hatua ya kuwahoji wahusika ambao walitoa sababu mbalimbali zilizopelekea utofauti wa majina yao ikiwemo sababu ya kubadili dini, na kuongeza kuwa suala hili liko nje ya uwezo wa Taasisi yake na ameliwasilisha kwa Katibu Mkuu-UTUMISHI kwa ajili ya hatua stahiki.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Dkt. Laurean Ndumbaro, Katibu Mkuu-UTUMISHI amesema anaamini kuwa waajiri wameshawaondoa katika Orodha ya Malipo ya Mishahara ya Serikali (payroll) watumishi wote waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi kuanzia awamu ya kwanza hadi ya tano ya uhakiki, isipokuwa waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi katika awamu ya sita iliyotolewa leo.

Kuhusu watumishi 1,907 ambao hawajawasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kuhakikiwa, Dkt. Ndumbaro amesema Mhe. Rais au Mamlaka yoyote inayotambulika kisheriakatika Utumishi wa Umma inapotoa maelekezo au maagizo na wanaotakiwa kutekeleza wasipotekeleza maagizo yaliyotolewa wanakuwa wametenda kosa la kutotekeleza maagizo halali kwa mujibu wa Kanuni, Sheria na Taratibu za Utumishi wa Umma kwa kukaidi maelekezo na maagizo ya Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kutokana na kosa hilo Dkt. Ndumbaro amewaagiza waajiri kuwachukulia hatua watumishi hao.

Dkt. Ndumbaro amesema kuhusuwatumishi 71 ambaomajinayao halisi ni tofauti na yaliyopo katika vyeti vyao walivyotumia kujipatia ajira katika Utumishi wa Umma yatawasilishwa kwenye vyombo vya Dola vyenye mamlaka ya kufanya uchunguzi na kutoa taarifa itayotoa maoni na ushauri wa hatua za kuchukuliwa. Aidha,watumishi 295 waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi katika uhakiki wa awamu ya sita iwapo hawataridhika na matokeo ya uhakiki wanapewa fursa ya kukata rufaa hadi tarehe 31 machi, 2018.

Katibu Mkuu, Dkt. Ndumbaro amewashukuru wananchi na watumishi wa umma ambao wametoa taarifa za uwepo wa watumishi wenye vyeti vya kughushi Serikalini na kuwaomba kuendelea kutoa taarifa za watumishi wengine wasio na sifa kupitia namba yake ya simu ya kiganjani 0754 261 965 ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais za kuwa na watumishi wa umma wenye sifa stahiki.

Dkt. Ndumbaro amesema kuwa pamoja na kuwa, zoezi la uhakiki lililofanyika, Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa wameelekezwa kufanya ukaguzi wa majadala ya watumishi waliochini ya Ofisi zao ili kujiridhisha kama watumishi waliobakia wana sifa stahiki na ukaguzi huo ufanyike hadi kufikia tarehe 25 Machi, 2018. Aidha, amesisitiza kuwa, baada ya tarehe 25 Machi, 2018, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora itafanya ukaguzi wa kushtukiza katika baadhi ya Ofisi na Taasisi za Umma ili kujiridhisha na namna zoezi la uhakiki livyofanyika kwa Waajiri wote katika Utumishi wa Umma.

Pamoja na maelekezo hayo, Dkt. Laurean Ndumbaro ameeleza kuwa Serikali inaandaa utaratibu wa kuhakiki vyeti vya Taaluma vinayotolewa na vyuo vya elimu ya Juu vya ndani na nje ya Nchi. Aidha, Watumishi walisoma vyuo vya nje ya nchi, watapaswa kuviwasilisha Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania – TCU ili vihakikiwe kujiridhisha na uhalali wa vyeti husika.